CHAKULA CHA WASHINDI no05

“UPAKO WA KUFANYA ZAIDI YA WENGINE”

Na Mwl Dickson Cornel Kabigumila.

2Wafalme 4

2Wafalme 4

“Basi palikuwa mwanamke fulani, mmoja kati ya wake wa wana wa manabii aliyemlilia Elisha, akisema: Mtumishi wako, mme wangu, amekufa; nawe unajua vema kwamba mtumishi wako alikuwa mcha Mungu. Na mkopeshaji amekuja kuwachukua watoto wangu wawili wawe watumwa wake. Kwahiyo Elisha akamwambia: Nikufanyie nini? Niambie; Una nini nyumbani mwako? Naye akamjibu: Mjakazi wako hana kitu chochote nyumbani ila chupa ndogo ya mafuta. Ndipo Elisha akasema: Nenda ujiombee vyombo kutoka nje, kutoka kwa jirani zako wote, vyombo vitupu. Usijizuie kwa kuchukua vichache. Nawe uende ufunge mlango nyuma yako na wana wako, nawe umimine katika vyombo hivyo vyote, na uweke kandoo vilivyojaa. Basi akaenda zake kutoka kwake.
Alipofunga mlango nyuma yake na wanawe, wakawa wakimletea karibu vile vyombo, naye akawa akimimina. Na ikawa kwamba mara tu baada ya vyombo vile vilipojaa, akamwambia mwana wake: Niletee karibu tena chombo kingine. Lakini akamwambia: Hakuna chombo kingine. Ndipo yale mafuta yakakoma. Kwahiyo akaingia na kumwambia yule mtu wa Mungu wa kweli, naye sasa akasema: Nenda uza hayo mafuta ulipe madeni yako, nawe pamoja na wana wako mtaishi kwa kile kitakachobaki” (2Falme 4:1-7, New World Translation, Swahili).

Mambo ya kujifunza:

1. “Ni muhimu kwa kila maamuzi unayofanya kufikiri pia kuhusu athari au madhara watakayopata wengine wanaokuhusu kutokana na kile unachokifanya leo”

Kwenye habari hii tunaona kuwa huyu ndugu alikopa na kuwa na deni, lakini madhara ya deni yalikuja kuwapata mke na watoto wake ambao hawakukopa na hawakuhusika kuchukua huo mkopo.
Haijalishi alichukua mkopo na kuutumia kwa maendeleo au la! Ninachokiongelea ni matokeo ya maamuzi yake, yaliwapata watoto wake ambao hawakwenda kujiingiza kwenye madeni.
Kumbuka hili: Kila jema au baya unalolifanya leo ni mbegu. Usipolivuna wewe binafsi, watalivuna wanao.
Ni muhimu kupata muda wa kutafakari, kuomba na kupata ushauri wa kina toka kwa wenye Mungu kabla ya kuchukua mkopo au kujiingiza kwenye madeni.
Biblia inasema Elisha alikuwa anamjua huyu nabii aliyefariki, na mkewe alimwambia Elisha: “Nawe unajua ya kuwa mme wangu alikuwa akimcha Mungu”…
Ninachoshangaa hapa ni hiki: Huyu mwanaume hakuja kwa Elisha kuomba ushauri kabla ya kuchukua mkopo, lakini alipokufa mkewe (mwenye hekima) akaja kwa mtumishi wa Mungu kutafuta suluhu.
Kama angelikuja kwa Eliya kabla ya kukopa, ninaamini Mungu huyuhuyu aliyeyaongeza mafuta ya chupa kufuta deni angeweza kutumia “walichonacho” kingine kuwapa muujiza na wasingeingia kwenye madeni.
Kumbuka hili: Maamuzi unayofanya leo, utapata matokeo yake siku moja, iwe moja kwa moja kwako au kwa wanao kama huyu nabii aliyekufa na deni.
Utie moyo wako hekima na ufahamu kabla ya kufanya maamuzi. Tafuta uso wa Mungu au katafute hekima kwa Mtu wa Mungu wa kweli unayemjua yuko vizuri na hekima ya Mungu imejaa ndani yake!

2. “Adui anaziona fursa za kukutoa kwenye jaribu au pito ulilonalo na anafanya kila awezalo akunyang’anye hizo fursa”

Huyu mdeni (naweza kumwita adui) aliona “fursa” kupitia watoto wa huyu mwanamke mjane. Yeye aliwaona kama “rasilimali” inayoweza kutumiwa kuzalisha kile anachodai.
Lakini huyu mama yeye aliishia kuwaona wale watoto kama watoto tu, hakuwaona kama fursa ya kumaliza deni.
Angeweza kushirikiana nao kufanya vibarua, shughuli za uzalishaji nakadhalika na kuweza kupata pesa ya kulipa deni. Lakini yeye hakuwaona kwa jicho la “rasilimali” tofauti na yule mdeni alivyowaona.
Ndugu yangu, kuna vitu vingi ulivyonavyo ni “rasilimali” na vimebeba “fursa” za kigeuza jumla maisha yako, na ndio maana “adui” amekuwa akikuzuia “usivifanyie kazi” japo moyoni mwako unaona vinaweza kugeuza maisha yako au kukusogeza mahali.
Wengine mmevitumia kwa kiwango cha chini, yaani mmevichukulia tu kama “hobby” au kama “starehe” au kitu cha kujifurahisha tu!
Hata Lionel Messi na Christiano Ronaldo wanaucheza mpira wa miguu kama “hobby” na kama “leisure” lakini wamejipambanua na kwenda hatua ya ziada na kukitumia hicho kama “rasilimali” na wanalipwa mamia ya mamilioni kila wiki kwa kitu ambacho wanakifanya kwa raha na bila kutumia jasho jingi.
Mimi napenda kufundisha wengine. Napenda kumsaidia mtu atoke mahali na niweke alama maishani mwake. Ni kitu nafanya bila kutoa jasho. Najua thamani yake, najua ni kipawa kinachoweza kunikutanisha na wakuu. Naelewa kinaweza kunitengenezea nafasi. Hivyo nakifanyia kazi kwa moyo wote na nikiwa na picha kubwa na msukumo wa kuyagusa maisha ya mamilioni kwa hekima na ufunuo alioweka Mungu maishani mwangu.
Nawe una “watoto” ambao mdeni (adui) anataka kukunyang’anya na kuwapeleka utumwani… Ni uamuzi wako kuwatuma wakuletee vyombo ufanye muujiza utokee au uwaache wachukuliwe!
Chochea kipawa chako…. Fanyia kazi hayo mawazo yanayozaliwa ndani yako… Ukiyaacha yanaelea, adui atakuibia.
Anza kufanyia kazi hicho kilichozaliwa moyoni mwako… Tutafute watumishi wa Mungu tukushauri na tukuelekeze namna ya kukifanya halisi… Usikubali kichukuliwe na mdai wako!

3. “Hakikisha una ukaribu na urafiki na watumishi wa kweli wa Mungu”
Nakupa ushauri huu na kama utauzingatia kuna siku utanikumbuka.
Kilichomwokoa na kumsaidia huyu mwanamke ni uhusiano aliokuwa nao na Mtu wa Mungu Elisha.
Biblia inasema, Elisha alifahamiana na mmewe. Hivyo hawakuwa wageni kwake, na wakati wa magumu walipata msaada walioutaka!
Ni kweli wote tumeokoka na tunaweza kuomba na kujibiwa na Mungu lakini kubali au kataa, kuna upako na mafuta ya tofauti na ya ziada kwa mtumishi wa Mungu wa kweli ambayo yanatosha kukusaidia na kukutoa kwenye jaribu lako!

4. “Mara nyingi matatizo na majaribu yanayotujia, huwa yanakuja kwetu tukiwa tayari na mlango wa kutokea”

Huyu mwanamke jaribu lilimjia kama yanavyotujia sote. Lakini rasilimali za kumtoa kwenye mateso yake alikuwa nazo. Alikuwa na watoto ambao walikusanya vyombo na kumsaidia kuuza mafuta. Alikuwa na chupa ya mafuta ndani iliyotumika kuzaa muujiza. Alikuwa na majirani wazuri (watu sahihi) waliompa vyombo vitupu. Alikuwa na imani iliyompeleka kwa mtumishi wa kweli wa Mungu na pia kuwa tayari kutii kile alichoelekezwa bila kuangalia au kujiuliza kama kina “make sense” au la. Na alikuwa anafahamiana na mtumishi wa kweli wa Mungu mwenye majibu yake.
Mara nyingi ukiangalia katika yote uliyopitia, utagundua kila jaribu, gumu, changamoto au tatizo lilipokujia, rasilimali za kukuvusha zilikuwa karibu nawe.
Hii ndio kanuni ya Mungu… Huwa haruhusu tupitie jaribu lililo nje ya rasilimali tulizonazo… Changamoto pekee ni kujua namna ya kuzitumia tu kwa usahihi!

5. “Usimsahau mtumishi wa Mungu aliyekusaidia kuvuka ulipokuwa unapitia”

Hili ni jambo la muhimu sana. Lakini wengi wetu tunalikiuka.
Watu wengi wakiwa na shida na magumu ni wepesi wa kukimbilia kwa watumishi wa Mungu lakini “mambo yakijipa” hawarudi, kama wale wakoma tisa walioponywa na Bwana Yesu.
Utakuwa mjanja kwa muda, lakini Mungu ataruhusu jaribu na changamoto nyingine na utamhitaji tena huyu mtumishi uliyempuuza na kumsahau juzi.
Nakushauri: Kama kuna mtumishi wa Mungu alikusaidia kuvuka pito lako fulani, mshike vizuri, Mungu amempa majibu yako, kaa naye vizuri… Kula naye karibu!
Kama kuna mtumishi wa Mungu alikuombea au kukusaidia kuvuka mahali na haujarudi na ushuhuda au shukurani kwa Mungu wake aliyekusaidia, leo nakusihi urudi na ukamuone.
Biblia inasema, huyu mwanamke mjane alipoona mafuta yamejaa vyombo, alirudi kwa Elisha na huko alipata “maelekezo” ya namna ya kuutumia “muujiza wake” wa mafuta kukomesha deni alilokuwa anadaiwa pamoja na kutunza familia yake.
Mwenye masikio na asikie.

Na hiki ndicho chakula cha washindi leo,
Umebarikiwa,
Mwl D.C.K

Advertisements

Karibu kwenye Tovuti ya Kikristo... hapa utapata mafunzo Mbali mbali ya kukujenga kiimani ,kifahamu,kimazingira na hata kitabia Karibu Tena

Tagged with: , ,
Posted in Mafunzo

Toa mawazo,maoni

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

yaliyopita
Ungana nasi kwenye kurasa yetu  ya facebook na like page yetu-kuweza kutangaza neno la bwana na utabalikiwa sana..kwa kazi yako kuu kwani thawabu yako mbinguni ni tele

Andika E-mail kwenye box hapo chini kisha Bonyeza (jiunge Hapa)na uweze kujiunga na tovuti hii kupitia e-mail yako utakayojisajilia,tutaweza kukupa kila taarifa,habari zinazojili kwenye hii blog yetu asanteni

Join 2,219 other followers

Upcoming Events

No upcoming events

%d bloggers like this: