CHAKULA CHA WASHINDI no07

“UPAKO WA KUFANYA ZAIDI YA WENGINE”

Na Mwl Dickson Cornel Kabigumila.

Wakoma

“Basi palikuwapo watu wenye ukoma, penye lango la mji; Wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe? Tukisema tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vilevile. Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami; Wakituhifadhi hai tutaishi; Wakituua, tutakufa tu. Basi wakaondoka kabla ya mapambuzuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na walipofika mwanzo wa kimo cha Washami, kumbe! Hakuna tu. Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi. Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kimo chao vilevile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao. Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja, wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha; wakarudi, wakaingia hema ya pili, vilevile wakachukua vitu, wakaenda wakavificha. Ndipo wakaambiana, mambo haya tufanyayo si mema; Leo ni siku ya habari njema, na sisi tunanyamaza; mkingoja hata kutakapopambazuka, madhara yatatupata; Basi twende tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme” (2Falme 7:3-9).

Mambo ya kujifunza:

1. “Kama unataka kutoka ulipo au kubadili hali yako ya kimaisha; Jizoeze kujiuliza maswali”

Hawa wakoma wanne waligeuza hali yao ya maisha kwa njia hii.
Walijiuliza maswali na kujitathmini kuhusu kiwango chao cha maisha walichonacho, na ulazima wa kutoka hapo, Hatari za kuendelea kukaa hapo walipo, hatari ya kuamua kuchukua maamuzi ya kuondoka hapo walipo na wakagundua kila kitu kilikuwa hatari kwao, lakini hatari zilitofautiana kiwango cha madhara.
Kuendelea kubaki walipokuwa ilikuwa hatari, kutoka walipo kuelekea walikoona neema nayo ilikuwa hatari… Lakini pia walijihoji juu ya faida zilizomo ndani ya hatari zote mbili. Na mwisho wa siku wakachukua maamuzi ya kutoka walipo kuelekea mlango wenye neema zaidi.
Asikudanganye mtu: Kila mlango wa neema na baraka una vita vikubwa na upinzani.
Kanaani ilikuwa nchi ya maziwa na asali lakini ilikuwa na majitu.
Kupata mamlaka yote duniani na mbinguni na kuzimu kwa Bwana Yesu ulikuwa mlango mkubwa na wa kufaa lakini kulikuwa na hatari ya msalaba, mauti, kaburi na aibu kabla ya utukufu.
Hakuna njia ya neema kwenye Ufalme wa Mungu iliyo wazi, lazima utumie imani, upako na neema kuwahamisha majitu.
Ni lazima upuuze msalaba, aibu, mauti na kaburi ili ukirimiwe jina kuu lipitalo majina yote.
Hata mti kabla haujawa mti mkubwa lazima ukubali kuanza kama mbegu… Ianguke chini na kufa… Halafu uhai na utukufu huchipuka na kukua na kukua na kudhihirika kwa kila mtu hatimaye!

2. “Upungufu au udhaifu ulionao si hasara bali ni kigezo cha Mungu kudhihirisha utukufu wake kupitia wewe”

Hawa walikuwa wakoma… Daudi alikuwa mchunga kondoo, mdogo, mzuri wa uso, asiyeujua uongozi, asiyezijua mbinu za kijeshi wala kutajwa miongoni mwa Wana wa Yese wenye bright future. Rahabu alikuwa kahaba maarufu kule Yeriko. Musa alikuwa na kigugumizi na muuaji. Paulo alikuwa mtesi wa kanisa na muuaji. Petro alikuwa mvuvi asiye na elimu. Yabezi alikuwa na historia mbaya na alikuwa wa familia duni.
Lakini wote hawa na wengine wengi wana historia kwenye Biblia yako.
Mungu tunayemwabudu ni Mungu anayetumia vitu vipumbavu vya dunia hii ili aviaibishe vyenye hekima.
He does not call the qualified but He qualifies the called.
Si wenye mbio washindao… Si wenye hekima ya dunia hii wang’aao… Mungu huwanasa wenye hekima ya dunia hii katika hekima yao!
Si wengi walio bora wala walio wenye heshima waitwao… Haijalishi una mapungufu kiasi gani na kasoro nyingi ambazo hazikupi haki ya kuwa kwenye nafasi ya kuwa Mfalme… Ikiwa utausafisha moyo wako na kuwa sawa mbele za Mungu, utawabwaga wote wanaopigiwa chapuo kukushinda!
“Mungu si kama wanadamu, wao huangalia nje, lakini yeye huangalia moyo”

3. “Mungu ana malighafi zote zinazohitajika kuzalisha muujiza unaoutaka”

Biblia inasema Mungu aliwasikizisha wakoma vishindo.
Vishindo vya miendo ya magari, vishindo vya farasi, vishindo vya jeshi kubwa… Hivi vishindo vyote vitatu, Mungu alikuwa navyo kwenye “maktaba” yake mbinguni muda mrefu hata kabla jaribu na tatizo halijaja!
Ninakuhakikishia mwana wa Mungu: Mungu ana kila malighafi ya kuzalisha muujiza wako unaoutaka… Chukua hatua ya imani kama wakoma wanne… Halafu utashangaa ukifika kwenye kambi ya adui zako hautawakuta… Watakuwa wamekimbia na kukuachia, chakula, maji na utajiri mkubwa!
Usiogope jaribu au changamoto inapokuja maishani mwako… Mungu tayari anazo “audio” za kuwasikizisha adui zako!

4. “Ni tabia ya Mungu kuliruhusu likujie, lakini huwa analipumbaza linakuja na mali zote lilizonazo, ukilishinda tu, linageuza maisha yako”

Hakukuwa na sababu kwa mtu anayekwenda vitani kuja na dhahabu, fedha na mavazi ya gharama.
Lakini Mungu alihakikisha Washami “wanapumbazwa” wanakuja na “utajiri wao wote” kwenye uwanja wa vita!
Waliposambaratishwa na Mungu wa Wakoma, utajiri wao na chakula chao vikatekwa nyara.

Ushauri wa bure: Kwa kila jaribu, tatizo au ugumu utakaopitia, usiangalie upande hasi tu wa namna unavyosongwa…. Angalia utukufu unaokungoja kama utavipiga vita vizuri vya imani.
Heri yeye ashindaye NITAMPA…. Hii ni ahadi ya Bwana Yesu!
Kwa kila unachokishinda atakupa… Ukishinda kidogo, reward yako ni ndogo nakadhalika.
Nyuma ya kila Goliati kuna Ufalme unakusubiri.
Nyuma ya kila jitu kuna nchi ya maziwa na asali.
Nyuma ya kila msalaba, mauti na kaburi kuna ufufuo na jina kuu lipitalo majina yote.
Chukua fursa, twende zetu!

5. “Kila utakapokula, kunywa, kupata fedha, dhahabu na maisha yako kugeuka; Usiwasahau watu wa nyumba ya mfalme”

Wale wakoma walipoona kila kitu kimewaendea sawa hawakujenga vibanda na kuanza kuringa na mali. Bali walirudi na kuwapasha habari watu wa nyumbani kwa Mfalme.
Hiki ndicho tunachopaswa kufanya kama watu waliookoka. Kila Mungu akitupatia baraka, ustawi na hatua kubwa ya kimaisha, tusiwasahau “watu wa nyumbani kwa Mfalme (waliookoka walio katika hali ngumu na uhitaji)”
Ukipata biashara yako, ikakua na kuongezeka, usiwasahau watu waliookoka waaminifu walioko nyumbani kwa mfalme.
Mungu akikupa fursa za kueleweka za kimaisha, Fanya kama wale wakoma wanne… Usiwasahau watu wa nyumbani kwa Mfalme!

Na hiki ndicho chakula cha washindi leo,
Umebarikiwa,
Mwl D.C.K
www.yesunibwana.org

Advertisements

Karibu kwenye Tovuti ya Kikristo... hapa utapata mafunzo Mbali mbali ya kukujenga kiimani ,kifahamu,kimazingira na hata kitabia Karibu Tena

Tagged with: ,
Posted in Mafunzo

Toa mawazo,maoni

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

yaliyopita
Habari iliyotazamwa sana
Ungana nasi kwenye kurasa yetu  ya facebook na like page yetu-kuweza kutangaza neno la bwana na utabalikiwa sana..kwa kazi yako kuu kwani thawabu yako mbinguni ni tele

Andika E-mail kwenye box hapo chini kisha Bonyeza (jiunge Hapa)na uweze kujiunga na tovuti hii kupitia e-mail yako utakayojisajilia,tutaweza kukupa kila taarifa,habari zinazojili kwenye hii blog yetu asanteni

Join 2,215 other followers

Upcoming Events

No upcoming events

%d bloggers like this: