CHAKULA CHA WASHINDI No08

UPAKO WA KUFANYA ZAIDI YA WENGINE

Na Mwl Dickson Cornel Kabigumila.

https://yesunibwana.files.wordpress.com/2015/02/05cf0-mark1fishersofmenpicture.jpg?w=605“Ikawa makutano walipomsonga wakisikiliza Neno la Mungu, yeye alikuwa amesimama kando ya ziwa Genesareti, akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu zao. Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni. Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mkavue samaki. Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; Lakini kwa Neno lako nitazishusha nyavu. Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika. Wakawapungia mkono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, maana mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana. Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata; na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu. Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata” (Luka 5:1-11).

Mambo ya kujifunza:

1. “Kila mahali Neno la Mungu linapohubiriwa kwa usahihi, lazima miujiza itokee”

Hiki ndicho kilichozalisha miujiza kwenye huduma ya Yesu.
Biblia inasema, “Watu walokuja kusikiliza na kuponywa”
Kila mahali Neno la Mungu linapofundishwa kwa usahihi, lazima uweko udhihirisho wa nguvu na Roho mtakatifu kuthibitisha kile kilichofundishwa.
Kila alipokwenda Yesu, alifundisha kwanza, ili kujenga imani ya wanaomsikia, halafu imani yao ilipokua ikikua, ndipo miujiza ilipoanza kutokea.

Mitume nao walifanya kazi kwa namna hii.
Biblia inasema, walitoka, wakazunguka “wakihubiri Neno” kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile Neno (walilohubiri) kwa ishara zilizofuatana nalo (Marko 16:20).

Hiki ndicho kinakosekana kwenye makanisa yetu.
Kuna madongo, vijembe, kuumbuana, kupigana nyundo, kutungiana jumbe badala ya kuhubiri na kufundisha Neno. Matokeo yake hakuna imani ya kutosha kuzalisha miujiza.
Wakitokea wanaohubiri na kufundisha Neno na ishara na miujiza ikaanza kutokea, Utawasikia wale wenye “makanisa machovu” wakiwaambia washirika wao: Msifuate miujiza!
Au “Miujiza ni kwa wasioamini, si kwa sisi tuliokwisha kuokoka”
Huu ni uongo wa Ibilisi… Kila Yesu alipokuwa akimaliza kufundisha na kuhubiri, Miujiza ilitokea!
Mitume walipokuwa wakimaliza kufundisha na kuhubiri Neno miujiza ilikuwa ikitokea.
Mimi nikihubiri na kufundisha Neno kwa usahihi, miujiza itatokea.
Wewe ukifundisha au kuhubiri Neno kwa usahihi, miujiza itatokea.

Hatuwezi kuikwepa miujiza. Hatuwezi kujitenga na miujiza.
Ukristo bila miujiza utakuwa dini kama dini nyingine.
Biblia inasema, “Iko miujiza mingi sana ambayo Yesu alifanya ambayo hata tungeifanya dunia iwe karatasi, isingelitosha kuiandika” na Mungu hawezi kutia chumvi, ni kweli!
Yesu alikuwa mtu wa miujiza… Aliwaza miujiza… Aliongea miujiza… Alipumua miujiza…. Alitenda miujiza!
Lazima kanisa lirudishe miujiza… Hiki ndicho kitambulisho cha waaminio… Ni ishara au dalili ya kumtofautisha mwamini na asiye mwamini.
“Ishara hizi zitafuatana nao waaminio… Watatoa pepo…. Wataweka mikono juu ya wagonjwa wa namna zote nao watapata afya… Watakunywa vitu vya kufisha lakini havitawadhuru… Watajazwa na Roho mtakatifu na ushahidi wa nje wa kunena kwa lugha utakuwa dhahiri!
Kinachokwamisha miujiza isitokee ni taratibu za ibada na mipangilio ambayo haikuwepo wakati wa Yesu… Kama Neno la Mungu linapewa nafasi kidogo… Linahubiriwa na kufundishwa na watu ambao hawaamini miujiza…. Wanaowasema watumishi wengine wa Mungu madhabahuni… Hautatokea muujiza hata wa mafua kuponywa!
Miujiza ni matokeo ya kuhubiriwa na kufundishwa kwa usahihi Neno la Mungu, lazima watu watarudi na shuhuda!
Petro na wenzake walipolisikia Neno lililozalisha imani ndani yao walipata samaki kiwango cha “nyavu kuchanika” na “boti kuzama” (Net bursting and ship sinking amount)!

2. “Mabadiliko yanatoka nje ya mfumo”

Petro na wenzake walikuwa na mfumo wa uvuaji walioujua na kuutumia wavuvi wote… Samaki huvuliwa usiku kukiwa na giza na si mchana!
Lakini mfumo huu ulipokwama ilihitajika nguvu toka nje ya mfumo huu wa kibinadamu ili kuweza kupata samaki tena.
Petro alielewa siri hii… Akakubali kubadilika na kutumia kitu kingine nje ya akili na hekima ya kibinadamu… “Kwa Neno lako nitazishusha nyavu” bila kujali akili yangu inakubali au la…. Marafiki na ndugu zangu wananielewa na kuniunga mkono au la… Ila kwa Neno lako nitazishusha nyavu!

Wakati Jeshi la Washami lilipouzingira mji wa Yerusalemu, Waliouokoa mji na waliotumiwa na Mungu kuleta mabadiliko ni wale WAKOMA WANNE WALIOKUWA NJE YA MJI (Nje ya Mfumo)!

Mungu alipotaka kuleta ukombozi kwa Israeli, Walipokuwa wametekwa na Goliati na Jeshi lake kwa siku 40 mfululizo, alitumia kijana “toka nje ya kambi, nje ya jeshi (nje ya mfumo)” aitwaye Daudi!

Mungu alipotaka kuupiga Yeriko na kuutia mikononi mwa Israeli, Alimtumia mtu “nje ya Wana wa Israeli (mtu nje ya mfumo)” kahaba Rahabu!

Kila mabadiliko makubwa hutokea nje ya mfumo… Pale mfumo unapokosa majibu, ni wakati mzuri wa kumgeukia Mungu na Neno lake!
Inawezekana yako mengi umetumia elimu, ujuzi, mbinu na akili za kibinadamu kuyafanya kama wafanyavyo wengine na kufanikiwa lakini haujapata mafanikio kama ulivyotarajia… Ni wakati wa kumjia Mungu, na kulitumia Neno lake kabla ya kutupa tena nyavu!

3. “Ukitaka kuuona uwepo na utenda kazi wa Yesu: Mpe chombo chako”

Kilichomfanya Yesu amfikirie Petro na biashara yake iliyokuwa imekufa ni sadaka aliyoitoa ya chombo chake kitumiwe na Yesu kupeleka injili!
Kama Petro angelimnyima Yesu chombo chake, Yesu angekwenda kwenye chombo cha mwingine aliye tayari na angemfanyia huyo muujiza!
Ukimtaka Yesu kwenye biashara yako… Mpe Yesu chombo chako ahubirie injili.
Ukimtaka Yesu kwenye ndoa yako… Mpe Yesu chombo chako ahubirie injili.
Ukimtaka Yesu kwenye elimu yako… Mpe Yesu sadaka ya chombo chako ahubirie injili.
Ukimtaka Yesu ofisini kwako… Mpe chombo chako ahubirie injili!

Siri: Sadaka inayohusiana moja kwa moja na kitu unachotaka Yesu aje kukigeuza hiyo ndiyo itakayomleta Yesu hapo.
Petro alitoa chombo chake cha kazi kabla ya kumuona Yesu anayeleta samaki mchana kweupe!

Mwanamke mjane wa Sarepta alikuwa amebakiza chakula mlo mmoja ale na mwanae kisha wafe… Lakini alipompa Mungu nafasi ya kula chakula chake kupitia nabii Eliya… Kapu lake halikuishiwa unga wala mafuta hayakukoma!

Mwanamke Mshunami alipojua namna ya kumuingiza Mungu nyumbani kwake… Alimjengea chumba Elisha na kumlisha chakula… Mwisho wa siku alipata mtoto… Hata alipokufa, Mungu alimfufua tena!

Kornelio na nyumba yake walijua siri hii… Waliwapa watu sadaka nyingi na kuomba kwa bidii mpaka Mungu akashindwa kuvumilia…. Akawaokoa na kuwajaza Roho mtakatifu!

Dorcas/ Thabita alijua siri hii… Alitumia taaluma yake na biashara yake ya ushonaji kuwavika wajane… Hata alipokufa, sadaka yake iliongea mbele za Mungu akaishi tena!

Kama unamtaka Yesu kwenye jambo lolote… Mpe chombo chako ahubirie injili… Toa sadaka maalum ya kusapoti injili ikiwa ni mahususi Mungu aguse hicho kilichokufa au kisicho na matunda!

4. “Haimsumbui Mungu kufanya muujiza wa samaki ambao Petro hatawauza wala kuwafaidi ilimradi anajua kwa muujiza huo atampata Petro”

Yesu anasema, thamani ya roho moja mbele za Mungu ni kubwa sana kiasi kwamba mali zote na ulimwengu wote na fahari zote haziwezi kulinganishwa na thamani ya nafsi ya mtu!
“Kwa maana itamfaidia nini mtu kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake? (Marko 8:36-37).
Mungu yuko tayari kufanya chochote ili tu amuokoe mwenye dhambi.
Yesu alitenda muujiza wa samaki wengi sana kuvuliwa siku ile lakini mwisho wa siku “waliachwa wote” baada ya kuipata roho ya Simoni Petro na wale wana wa Zebedayo!
Haimsumbui Mungu kufanya muujiza ilimradi huo muujiza utavuna roho ya mtu.
Thamani ya samaki ni ndogo mno kuliko roho ya Petro aliyoipata siku ile!
Mungu yuko tayari kufanya muujiza wowote “unaoutaka” ili kumuokoa mmeo/ mkeo,
Mungu yuko tayari kufanya muujiza wowote “unaoutaka” ilimradi utaleta roho ya mtu au watu kadhaa kwa Yesu!
Ni maombi yangu kwa Mungu, atende miujiza ya kushangaza na kugeuza mioyo ya wote unaowapenda ambao bado hawajaokoka!

Advertisements

Karibu kwenye Tovuti ya Kikristo... hapa utapata mafunzo Mbali mbali ya kukujenga kiimani ,kifahamu,kimazingira na hata kitabia Karibu Tena

Tagged with: ,
Posted in Mafunzo
4 comments on “CHAKULA CHA WASHINDI No08
  1. Elisha Daudi says:

    Amen nimebarikiwa sana na mafundisho haya ya Neno la Mungu, Mungu akuinue na kuing’arisha huduma yako kwa mataifa wote wajue ns kuitumia hii ‘lulu’ iliyoko ndani yako

  2. Twarindwa eliewaha says:

    Nimebarikiwa sana na mafundisho,mungu akutie nguvu

Toa mawazo,maoni

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

yaliyopita
Habari iliyotazamwa sana
Ungana nasi kwenye kurasa yetu  ya facebook na like page yetu-kuweza kutangaza neno la bwana na utabalikiwa sana..kwa kazi yako kuu kwani thawabu yako mbinguni ni tele

Andika E-mail kwenye box hapo chini kisha Bonyeza (jiunge Hapa)na uweze kujiunga na tovuti hii kupitia e-mail yako utakayojisajilia,tutaweza kukupa kila taarifa,habari zinazojili kwenye hii blog yetu asanteni

Join 2,212 other followers

Upcoming Events

No upcoming events

%d bloggers like this: