SIKU 30 ZA MIUJIZA NA MAAJABU. (SIKU 30 ZA MFUNGO).[Day27].

https://i0.wp.com/www.safety4sea.com/images/media/2014/agreement.jpg

31/01/2016.

“NGUVU YA MAPATANO (THE POWER OF AGREEMENT)”

Mapatano ni makubaliano kati ya watu wawili au zaidi ili kufanya jambo.
Pia yaweza kuwa makubaliano kati ya makundi mawili au zaidi ya watu kwa kusudi la kufanya jambo moja pamoja.

Kibiblia mapatano yanamfanya Mungu AJE.
Mapatano yanamfanya Mungu AINGILIE KATI KWA WEMA AU KWA UBAYA.
Mapatano yanaweza kumfanya MUNGU AJE MAHALI KWA AJILI YA KUBARIKI AU KWA AJILI YA KULAANI!

Kusudi la kukufundisha somo hili la mapatano ni ili kukusaidia UKUTANE NA NGUVU YA MUNGU YA BARAKA INAYOACHILIWA MAPATANO MEMA YAKIFANYIKA.
Na pia kukuepusha na hatari za ADHABU NA LAANA YA MUNGU PALE MAPATANO MABAYA YAKIFANYIKA.
Ni muhimu ujifunze na kudaka siri hizi na kuzitumia KUINGIA MAPATANO MEMA YALETAYO BARAKA na kuzitumia KUEPUKA MAPATANO MABAYA YALETAYO ADHABU NA LAANA YA MUNGU.

Muhimu:
“Mapatano yoyote humleta Mungu mahali yalipofanywa hata kama hakuwa lengo la kupatana kwenu. Na akija ni kubariki kama ni mema, na kulaani na kuhukumia adhabu kama ni mabaya”

“MAPATANO YOYOTE HUMLETA MUNGU MAHALI HAPO. IWE KUBARIKI AU KULAANI”

1. MAPATANO MABAYA.

i) Watu walipojenga mnara wa Babeli ili wasitawanyike juu ya nchi.

Mungu alipoumba Mbingu na nchi, alikusudia WATU WAZAANE WATAWANYIKE NA KUIJAZA NCHI (Mwanzo 1:28).
Mungu alitaka watu wakiongezeka wazaeni na kuijaza dunia (nchi) na si kukaa sehemu moja.

Lakini hawa watu baada ya gharika, chini ya uongozi wa Nimrodi WALIFANYA PATANO KINYUME NA TAMKO LA MUNGU;

“Wakasema, haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ILI TUSIPATE KUTAWANYIKA USONI PA NCHI”
(Mwanzo 11:4).
Haya ni MAPATANO MABAYA.
Mapatano yaliyo kinyume na Mapenzi ya Mungu (Neno lake kwamba tuzae tuongezeke na kuijaza nchi).

Jifunze kitu hapa:
Hawa watu WALIPATANA NA KUKUBALIANA, WAKAANZA KUJENGA WALA HAWAKUMUITA MUNGU, LAKINI MAPATANO YAO MBALI YA KWAMBA YALIKUWA MABAYA, YALIMFANYA MUNGU ASHUKE NA KUZUIA UJENZI WA MJI NA MNARA KWA KUWACHAFULIA LUGHA YAO.
(Mwanzo 11:5-9).
Hawakuomba, hawakufunga, hawakutoa sadaka, hawakuabudu wala kusifu LAKINI MAPATANO YALIMFANYA MUNGU ASHUKE!

ii) Mapatano ya kutengeneza ndama waliyofanya Waisraeli.

“Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka kutoka mlimani, WAKAKUSANYANA wakamwendea Haruni, WAKAMWAMBIA HAYA! KATUFANYIZIE MIUNGU ITAKAYOKWENDA MBELE YETU, KWA MAANA HUYO MUSA ALIYETUTOA KATIKA NCHI YA MISRI HATUJUI YALIYOMPATA”
(Kutoka 32:1).
Hawa watu walikusanyana WAKAPATANA WANAHITAJI MIUNGU MINGINE YA KUWAONGOZA na Haruni akakubali na kuwatengenezea ndama kama walivyotaka!
Matokeo yake:
Mungu ALISHUKA KWA HASIRA ILI AWAANGAMIZE.
Lakini Musa, alisimama mbele yake kwa toba, ADHABU NA LAANA ALIYOTAKA KUACHILIA MUNGU IKAONDOLEWA (Kutoka 32:7-14).

Umewahi kujiuliza MAPATANO YA FAMILIA KUFANYA MAMBO YA MILA HUWA YANAPELEKEA NINI?
Mbali ya adui kuifunga na kuimilki familia husika, lakini MUNGU HUACHILIA LAANA NA ADHABU KWA FAMILIA HIYO iliyogeuka mbali na MUNGU KUIENDEA MIUNGU MINGINE.

Umewahi kujiuliza zile familia zinazopatana kuita mganga nyumbani afanye mambo yake pale?
Au zile zinazopeleka familia kwa mganga awatengeneze?
Mbali ya mikataba na kuzimu, hupelekea hao watu KULAANIWA NA KUADHIBIWA NA MUNGU.
Hata wasipokufa basi kuna kiwango kingine cha maisha watakikosa na mkono wa Mungu hautakuwa upande wao.
Kama umetoka familia ya namna hii, UNALAZIMIKA KWENDA MBELE ZA MUNGU KWA TOBA ILI KUWANASUA NA MIKATABA YAO PAMOJA NA ADHABU YA MUNGU JUU YENU.

iii) Dathani, Kora na Abiramu.

Hawa watu watatu WALIPATANA na wakataka kumpindua Musa njiani.
Wakidai aliwaahidi maisha bora katika nchi ya maziwa na asali lakini hawaoni hayo maziwa wala asali.
Wakaukusanya mkutano wa Wana wa Israeli, na kuanza kuwashawishi wamgeuke Musa na kurudi Misri.
Matokeo:
Mungu ALISHUKA NA AKATOA ADHABU, WAKAFA WAO NA WAKE ZAO NA WATOTO WAO.
Ilibakia kidogo Mungu aue na Mkutano mzima wa Israeli lakini Musa alimuomba asiue Mkutano bali awaue WANAMAPINDUZI Dathani, Kora na Abiramu pamoja na kila aliye nyumbani kwao.
Ardhi ilifunuka na wakamezwa wakiwa hai.
(Hesabu 16 Yote).
Angalizo:
“Usikubali kujiunga na mapinduzi au uasi wowote dhidi ya Mtumishi wa Mungu hata kama unadhani ana makosa au haumuelewi. Haitakuathiri wewe tu, hata uzao wako watapata adhabu. Jichunge rafiki”

iv) Anania na Safira
Utazikuta habari zao kwenye kitabu cha MATENDO YA MITUME SURA YA TANO.
Hawa ni mke na mme WALIOPATANA KUTOA SADAKA YA KIWANJA.
Walipokiuza Shetani akawadanganya nao WAKAPUNGUZA KIASI NA KULETA PUNGUFU YA WALICHOKUWA WAMEKUSUDIA.
Matokeo:
Uwepo wa Mungu ulishuka na Wakafa wote siku hiyohiyo.
Usicheze na mapatano yoyote ya kumchakachua Mungu, HATA USIPOKUFA KIMWILI, utapoteza “maisha yako” kwa namna moja ama nyingine!

Una mchezo wa kupunguza kiasi cha sadaka kwa kisingizio una mambo mengi au yameingiliana?
Mungu anaheshimu kiapo na agano uliloweka kuwa utaitimiza nadhiri.
Usijitetee ukadhani atakuacha kwa sababu wewe ni mwamini wa Agano jipya hivyo Mungu hataangalia utoaji wako.
Hata Anania na Safira walikuwa watu wa agano jipya lakini MAPATANO YAO YA KUMUIBIA MUNGU YALIONDOA UHAI WAO.
Si lazima ufe ila unaweza kuharibu maisha yako ukiwa KANJANJA.

2. MAPATANO MAZURI

i)Watu wa Ninawi

Hawa watu waliletewa unabii na nabii Yona kuwa ndani ya siku 40 Mungu atauangamiza mji wao kwa sababu ya dhambi na maovu yao (Yona 3:4).
Walipopata taarifa hizi mbaya; WALIKUSANYANA WAKAPATANA NA KUFUNGA NA KUOMBA KUANZIA MDOGO HATA MKUBWA NA HATA MFALME WAO (Yona 3:5-9).
Mungu akasikia na kuondoa hiyo adhabu na hukumu juu yao.
(Yona 3:10).
Haya MAPATANO MEMA YALIMLETA MUNGU MJINI NINAWI NA AKAGEUZA ADHABU NA HUKUMU JUU YA MJI WAO.
Hata sisi tunaweza kufanya namna hii kwenye familia zetu na miji yetu mambo yanapokuwa hayaendi.
Mapatano haya yanaweza kutumiwa na familia au eneo lolote ambalo mambo hayaendi.

ii) Shedraka, Meshaki na Abednego.

Vijana hawa watu WALIFANYA MAPATANO YA HATARI ambayo yalikuwa yakitishia hatma ya maisha yao.
Waliweka msimamo kuwa hawatakubali kuisujudia sanamu ya Mfalme Nebukadreza hata kama itawagharimu uhai wao.
MAPATANO YAO YALIMFANYA MUNGU AINGIE KWENYE MOTO KUHAKIKISHA HAUWAUNGUZI WALA KUWADHURU.
Walipatana kutomuuza Mungu wao kwa ajili ya chochote hata kwa kifo.
(Soma Danieli 3).
Hawakumuita Mungu aje kwenye moto, lakini MAPATANO YAO YA KUTOABUDU MIUNGU MINGINE YALIMFANYA MUNGU AJE MZIMA MZIMA.

iii) Kanisa lilipoomba kwa ajili ya Petro.

Biblia inasema Mfalme Herode alimuua Yakobo ndugu yake Yohana. Kama haitoshi akaamua kumkamata Petro naye akiwa na kusudi la kumuua.
Lakini KANISA LIKAPATANA NA KUOMBA KWA AJILI YAKE KWA BIDII USIKU KUCHA.
Mapatano yao yalimsababisha Mungu amtume malaika ambaye alimtoa Petro gerezani usiku uleule.
Mungu alitenda muujiza si kwa sababu walikuwa na imani, hapana!
Maana hata alipokuja na kijakazi Roda akawaambia Petro katoka acheni kuomba walibisha wakimwambia ana wazimu.
Wangekuwa na imani wasingesema Roda ana wazimu, bali wangelisema “Tulitarajia hilo, mfungulie aingie”
Mbali ya kutokuwa na imani kwenye maombi yao, lakini MAPATANO YAO YALIFANYA MUUJIZA UTOKEE!
(Matendo 12:1-17).

Tujiulize kama Kanisa tungekuwa tunamng’ang’ana Mungu na kuombea chochote kwa mzigo na mapatano kama hawa Mitume, nini kingekuwa kinatokea?
Kanisa, ni muda wetu kurudi kwenye aina hii ya maombi izaayo miujiza kupitia mapatano!

Kwa leo inatosha,
Umebarikiwa.
WEWE NI MTU MKUU NA MBARIKIWA!

Advertisements

Karibu kwenye Tovuti ya Kikristo... hapa utapata mafunzo Mbali mbali ya kukujenga kiimani ,kifahamu,kimazingira na hata kitabia Karibu Tena

Tagged with: , , ,
Posted in Mafunzo
One comment on “SIKU 30 ZA MIUJIZA NA MAAJABU. (SIKU 30 ZA MFUNGO).[Day27].
  1. John Matiku says:

    Ubarikiwe mtumishi wa Mungu kwa Ujumbe mzuri, Mungu akubariki,

Toa mawazo,maoni

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

yaliyopita
Ungana nasi kwenye kurasa yetu  ya facebook na like page yetu-kuweza kutangaza neno la bwana na utabalikiwa sana..kwa kazi yako kuu kwani thawabu yako mbinguni ni tele

Andika E-mail kwenye box hapo chini kisha Bonyeza (jiunge Hapa)na uweze kujiunga na tovuti hii kupitia e-mail yako utakayojisajilia,tutaweza kukupa kila taarifa,habari zinazojili kwenye hii blog yetu asanteni

Join 2,215 other followers

Upcoming Events

No upcoming events

%d bloggers like this: